Friday, August 12, 2011

KAZI YA SIASA KWANZA, YA CHAMA BAADAYE.



Ni ukweli usiopingika kuwa katika kundi, jamii, na hata nchi yoyote ile ni lazima kuwe na chombo, taasisi au mamlaka ambayo itakuwa na jukumu la kuongoza jamii hiyo kwa niaba ya wanajamii wote. Hii ni kutokana na kwamba si rahisi wananchi au raia wote kuwa na nafasi na uwezo sawia wa kuongoza au kuamua, na hata wakipewa nafasi hiyo matokeo yake ni kujiamulia mambo au utaratibu wa maisha bila kuzingatia misingi fulani fulani ya muhimu kwa kuwa kila mmoja atataka kujinufaisha kwa nafasi hiyo ya kujiamulia mambo. Na hasa kama tujuavyo, binadamu tumeumbwa na asli ya ubinafsi na tukiachiwa kila mmoja wetu ajiamulie na kufuata utaratibu autakao, matokeo yake huwa ni athari na mmomonyoko kwa jamii hiyo husika. Na ndipo kukaonekana umuhimu wa kuwa na chombo chenye kuundwa na baadhi ya wananchi (wawakilishi) wachache kwa niaba ya jamii husika na kwa maslahi ya wanajamii hao kwa ujumla.
Chombo hiki huwa na mamlaka ya kusimamia ustawi wa jamii au nchi hiyo katika Nyanja mbalimbali kama vile Nyanja ya uchumi, elimu, utamaduni, afya, na kadha wa kadha. Chombo hiki huitwa serikali na aghalabu katika dunia ya sasa hupatikana kwa njia ya uchaguzi ambapo wananchi huchagua viongozi wao kutokana na uwezo, haiba na hata itikadi walizonazo na chama kinachoshinda ndicho huunda serikali.
Si lengo langu hasa katika makala haya kuelezea kwa undani kuhusu umuhimu au ufanyaji kazi wa serikali, bali nataka kunasibisha uhusiano na ulinganifu wa kazi zifanywazo na serikali, na hasa kupitia vyama vya siasa. Kila chama cha siasa popote pale kianzishwapo huwa na lengo la kukamata dola, ikiwa ndiyo kubwa zaidi kwa kuwa kushika dola ina maana ndio kuongoza nchi na kuamua mambo kwa kufuata sera na ilani inayokiongoza chama hicho husika. Uhai wa chama chochote cha siasa, pamoja na mambo mengine, ni wanachama na vikao. Chama cha siasa kikiweza kuwa na wanachama wengi kwa idadi na kwa ufanisi, na kikifanya vikao vya mara kwa mara kujadili changamoto na mipango mikakati basi nguvu na uimara wa chama hicho huongezeka na kuwa mtaji wakati wote na hasa katika kipindi cha chaguzi mbalimbali.
Katika Tanzania yetu ya leo baada ya kuruhusu mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na kufuatiwa na uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, vyama vya siasa vimezidi kuongezeka na hivyo kwa namna moja au nyingine kuimarisha na wakati mwingine kudhoofisha mfumo huu wa vyama vingi. Hapo awali na hata sasa tarajio kuu la mfumo wa vyama vingi ni kusaidia si tu kuleta ushindani kwa chama tawala na kuisimamia au kuikosoa serikali bali pia kuwasaidia wananchi kwa kuwapa majibu na njia za kukabiliana kutatua changamoto mbalimbali kwa pamoja kuanzia ngazi za chini mpaka za juu kwa kubuni njia mbalimbali hata kama vyama hivyo haviundi dola.
Kazi za chama chochote cha siasa kwa kawaida zipo mbili kuu, kazi za chama na kazi za siasa. Kazi za chama wakati wote ni zile zenye maslahi tu kwa chama husika na wanachama wake, na mara nyingi kazi hizi hutakiwa kufanywa na kufanikishwa kwa hali na njia yoyote ile hata kama itakuwa na athari kwa wengine. Kazi hizi za chama hufanywa na makada, watu ambao wamebobea, wanakielewa chama hicho nje ndani na wapo tayari kwa lolote na hata chama kikiporomoka watu hawa huwa wapo tayari kubaki ndani ya chama hicho cha siasa. Na mara nyingi kazi hizi huwa hazifanywi na watu ambao hawaelewi vyema itikadi, msimamo na hata utaratibu wa vyama hivyo. Kazi za Chama hujumuisha kuongoza, kuhakikisha kinaendelea kuwepo, na uamsho.
Kazi hizi hufanywa kupitia maandamano na uelimishaji wa wananchi kuhusu ubaya wa sera za wapinzani, kuhakikisha mikutano inajaa watu wa kutosha. Kazi hizi hutokana na itikadi ya chama na huusisha makada ambao huwa wamejengewa utaalamu ndani na nje ya chama hicho, kwa kifupi kazi hizi ni kwa ajili ya kujenga chama.
Kazi ya siasa kwa upande wake pia hujumuisha kuongoza, yani kwa ufanisi na kufikia malengo tarajiwa na yenye tija si tu kwa chama hicho chenye kuunda serikali bali pia kwa wananchi wote kwa ujumla na kwa usawa. Kazi hii ya siasa hukitaka chama cha siasa na hata serikali kuhakikisha kinatekeleza sera zake vyema katika kuwaletea watu maendeleo na hasa kutokana na vipaumbele vya Taifa vilivyopo.
Nchi yetu ya Tanzania na hasa wananchi wake ambao wanachangamoto nyingi na za muda mrefu hawahitaji sana kuona kazi hizi za chama zikifanyika zaidi ya zile za siasa, yani hawafarijiki kuona viongozi wao wakitumia muda mwingi kutatua matatizo ya vyama vyao au kuwatumia wananchi hawa kuviongezea umaarufu vyama hivyo kuliko kutumia muda zaidi kuwahudumia wananchi hawa. Ni dhahiri shahiri kwamba gharama za maisha zimepanda tena sana na wananchi wengi hawajapata fursa kamili na hii kusababisha wengi wao kuzidi kukata tamaa zaidi ya maisha kuliko kutafuta njia mbadala ya kujikwamua na hali ngumu hii.
Mzigo huu wa maisha magumu umeachwa kwa Mh. Rais Jakaya Kikwete pekee na kwa baadhi ya mawaziri wachache ambao kimsingi kwa uchache wao huu wanashindwa kuyatimiza yale mema wanayoyafanya au kutaraji yafanywe nao kwa niaba ya serikali na kwetu sisi wananchi kwa ujumla. Rais Kikwete kila wakati amekuwa na dhamira ya dhati kuwasaidia Watanzania kwa mipango madhubuti, lakini tukumbuke mipango madhubuti bila utekelezaji ni sawa na ndoto tena za mchana zisizotimia. Mipango hii iwekwayo katu haiwezi kutimia kama hakuna ushirikiano wa pamoja tena wa dhati na hasa itokeapo Watanzania wenzetu tena wenye ubinafsi wanapoamua kufanya hila na mbinu zisotija ili kukwamisha juhudi hizi na hasa inapotokea watendaji wetu wa serikali walioaminiwa na kupewa dhamana na Taifa wanaposhindwa kumshauri vizuri, kiuhalisia na hata kumsaidia Mh. Rais katika kutekeleza mipango na mikakati. Watendaji hawa wamemuacha Rais Kikwete akiwa mpweke na mkiwa zaidi ya yatima akihangaika peke yake kila kukicha, kutatua matatizo ya nchi na hata katika chama chake, na wamesahau msemo ule wa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.
Tatizo la Tanzania si CCM kama inavyoaminishwa, tuachane na propaganda zisizo za msingi na sasa tuutumie vyema  mfumo huu wa vyama vingi tulioukubali na kuubariki tutambue kuwa Watanzania wanakabiliwa na matatizo ya msingi kuliko vyama hivi vya siasa. Kazi hizi za chama leo zinatuaminisha kuwa maandamano na matamko ndio suluhisho la matatizo yetu, hivi ni kweli Watanzania tutakula na kuishi kwa maandamano haya yafanywayo na vyama vya siasa? Tena yasiyo na lengo zuri wala tija kwa Taifa? Tumemaliza uchaguzi wa 2010 na bado tungali tukitarajia kutimiziwa ahadi na maendeleo kutoka kwa wawakilishi wetu tuliowachagua na kuwaamini. Tatizo kubwa zaidi na ambalo kila siku linazidi kukua ni hili la Viongozi wetu hawa wa kisiasa na vyama vyao wanaposhindwa kutofautisha kazi hizi mbili, ya chama na ya siasa. Kinachotuunganisha sisi wananchi wa kawaida na viongozi wetu wa kisiasa ni kazi ya siasa na si ya chama. Tena nieleweke wazi kuwa matatizo haya ya Watanzania siye yanasababishwa kwa kiwango kikubwa na viongozi wetu hawa tunaowaamini ambao hawatumii muda wao vizuri.
Eti imekuwa ni mtindo sasa kila chama kikitoa tamko hata kama halina mashiko, ukweli na tija kwa taifa, basi Mh. Kikwete atatakiwa ajibu na akikaa kimya basi itaonekana si mchapakazi na hana uchungu na nchi. Ni kweli ili kujiimarisha vyama hivi vya siasa hutumia njia za maandamano wakati mwingine ili kuzungumza na wananchi na kuwaeleza namna ya kutatua matatizo yao, na si kuwapa watu siasa za chuki zenye lengo la kuwafanya watu wachukie serikali yao. Hawa CHADEMA wamekua wakiwatumia wawakilishi wetu (wabunge) kuzunguka nao sehemu mbalimbali na kutupotezea wasaa sisi wananchi kupanga mipango na wabunge wetu hawa. Hata kama ni wanachama wao lakini wajue sisi wananchi hatukuwachagua kwa itikadi zao bali kwa uwezo tulioona wanao.
Wanasiasa hawa hawakuja kwetu kusema kuwa watahakikisha nchi haitawaliki na kwamba watatumia maandamano kutatua kero zetu, kwa mtindo huu wanatupa shaka kila kukicha hakika. Mpaka tunajiuliza au ndio mbinu za kutukimbia huku majimboni? Wananchi tumewachagua  kwa kuwa tumewaamini hasa walipoonesha nia kwa kutuambia kuwa “wana uwezo, na wako tayari kututumikia.” Sasa ifike mahala watambue kwamba huu ni wakati wao wa kututumikia na kufanya kazi ya siasa kutuletea maendeleo na kazi za kuimarisha vyama vyao waachiwe watendaji wengine wa vyama, na kwa wale wawakilishi wetu wenye nyadhifa pia kwenye chama basi wajue tunahitaji watumie muda wao mwingi kutatua matatizo ya wananchi ambao kwa pamoja kuna washabiki wa vyama na tusiokuwa na itikadi yoyote ya chama na hatuna mpango wa kujiunga na chama chochote katika siku za usoni.
Wawakilishi hawa wanaozunguka na chama chao kila kukicha wakielezea matatizo yaleyale yanayofahamika bila kutoa majibu ya ufumbuzi wake na kutupandikizia chuki dhidi ya serikali yetu, hawana tija kwa Taifa letu hili na ni dalili ya kutukimbia wapiga kura wao. Nadhani wanaweza kukisaidia chama chao cha CHADEMA kwa kuleta maendeleo zaidi majimboni (kwa kuwa wao si serikali) kwa kuchukua changamoto zetu na kuwa daraja kati yetu na serikali kwa kuzifikisha changamoto zetu na kuzifuatilia. Watambue pia wamechaguliwa na watu wa itikadi tofauti na ni wajibu wao kututumikia sote bila kufanya mambo kwa dhana eti wamepigiwa kura na wanachama wao tu, kuthibitisha hili wafuatilie majimbo kama ya Iringa Mjini,  Kawe, Nyamagana, Ilemela, Arusha Mjini na mengineyo na watasadiki haya niyasemayo. Hebu tuchukue mfano wa Rais Obama wa Marekani, yeye ni Rais wa nchi na kiongozi wa serikali, si kiongozi wa chama chake cha Democrats lakini kama mwanachama anafanya kazi kubwa ya kisiasa kwa ajili ya chama chake na kama ataongeza uchumi wa Marekani atakuwa amefanya kazi nzuri ya kisiasa kwa chama chake. Na hasa ataweza kuwavutia hata wanachama wa Republican wazidi kuvutiwa na sera za Democrats na kukisaidia chama chake pia kujiimarisha zaidi kwa kazi hiyo ya kisiasa aliyoifanya ambayo itazaa mambo mawili kwa pamoja yani kuwawezesha wananchi na chama chake pia.
Waswahili waliobobobea walishasema kuwa “Siasa si hasa bali ni kisa na mkasa”, na haya tunayaona sasa yanatimia, na siku zinavyozidi kwenda ndivyo wananchi wengi zaidi wanavyozidi kupoteza imani na mvuto kwenye siasa kwa kuwa hawasaidiwi vyema na ndio maana wananasibisha siasa kama “kisa na mkasa” kutokana na watu kuitumia siasa vibaya kutafuta umaarufu na kueneza chuki kwa upande mwingine. Mfano wa hili umesadifu kwa idadi ndogo ya wananchi waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi mkuu uliopita, ambapo sababu kubwa ni hii ya wananchi kupotewa shauku na mvuto katika siasa japo wana uchungu na nchi yao.
Huu si wakati wa kampeni kama CHADEMA wanavyofanya sasa, serikali na vyombo vyake hasa msajili wa vyama vya siasa asiwaonee haya wanasiasa hawa. Wananchi wanateseka sana na wanawategemea wao kuwanusuru, na kama wana sera au ilani yao basi wasubiri mwaka 2015 kama watajaaliwa ili wakipata nafasi ndio wafanya haya wanayoyafanya (kutangaza ilani katika kipindi kisicho cha kampeni). Na kama kuna wanaofadhili au hata kuwatuma (maana si bure) kufanya nchi isitawalike wafuatiliwe na wananchi tujulishwe ili tuwe tukivinyima kura zetu vyama vya kutumika na wachache kama hivi.
Nchi hii ya Tanzania ni yetu sote na kila mmoja ana haki na stahili zake hivyo wananchi wote kwa ujumla, watendaji wa serikali, pamoja na wawakilishi wetu hawa wanasiasa, imefika mahala tumsaidie Rais wetu Kikwete amalize kipindi chake kwa ufanisi kwa kumshauri vyema na kuwajibika kwa kila mmoja wetu katika nafasi au uwezo alionao. Nchi ikiyumba hatutasema kashindwa Kikwete bali itakua ni kushindwa kwetu sote, Kikwete pekee si Tanzania, Tanzania ni sisi Watanzania pamoja na Rais Kikwete na CCM yake, CHADEMA, CUF, TLP na wengineo na washabiki wao. Hatukuumbwa kuwa Watanzania bila sababu, tusiwe watu wa propaganda zaidi na kuacha kazi hizi za chama zituondoe katika hoja zetu za msingi na changamoto zetu za asili eti tu kwa kuwa wachache kati yetu wana ajenda zao binafsi ziso tija kwa Taifa. Nchi kwanza, Vyama baadaye na hakika tuipiganie na kuilinda nchi yetu kwa kutimiza wajibu wetu kama wazalendo.

Mobile no: 0713 587 577

No comments:

Post a Comment